Mkataba TTCL na TANESCOShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Septemba 07, 2021 limeingia mkataba wa mashirikiano na Wizara ya Mawasiano na Teknolojia ya Habari, katika matumizi na ujenzi wa miundombinu ya mkongo wa Taifa kwa kutumia miundombinu ya umeme.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na Katibu Mkuu Wizara ya Teknolojia na Mawasiliano ya Habari, Dkt. Zainabu Chaula, yakishuhudiwa na Mawaziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano ya Habari Dkt. Faustine Andungulile.

Akiongea kabla ya kusaini makubaliano, Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema lengo la kushirikiana ni kuwepo kwa matumizi mazuri ya fedha katika uwekezaji wa miundombinu hiyo.

"Ushirikiano huu utatusaidia kuwafikia wananchi kirahisi zaidi, kuliko kila Taasisi kufanya kwa peke yake, lakini vile vile tutapata dhamani ya fedha ambayo Serikali inaitoa" amesema Dkt Mwinuka.

Ameongeza tukio la makubaliano ni muhimu kwa pande zote mbili kutokana na kuwa itamsaidia Mhe. Rais kutimiza azma ya kufikisha umeme na kufikisha mawasiliano kwa kila mwananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo kati ya TANESCO na Wizara ya Mawasiano na Teknolojia ya Habari, pande zote mbili zimepata majukumu ya kufanya.

"Siku ya leo tarehe 07 Septemba ni siku ya kumbukumbu kwa Taasisi zilizo chini ya Wizara zetu kuanzisha mashirikiano ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja iwe kwa umeme, iwe kwa mawasiliano " amesema Dkt. Kalemani.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewapongeza wataalamu kwa kufanikisha kuanza kwa ushirikiano kati ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo.

"Hiki tunachokifanya ni Mapinduzi makubwa ndani ya Nchi yetu katika eneo la mawasiliano, lakini vilevile tunafuata maelekezo ya Mhe. Rais wetu ya kutUtaka kuwa na ushirikiano wa karibu" Dkt. Ndugulile