Mjumbe wa Bodi TANESCOBaraza Kuu la 51 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limehitimishwa leo Desemba 17, 2021 Mkoani Morogoro ambapo kati ya maazimio sita makubwa waliyokubaliana ni kuunga mkono jitihada za serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha malengo ya shirika ya kuwa na umeme wa uhakika yanafikiwa.
 
Akifunga baraza hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, CPA Zawadia Nanyaro amesema TANESCO itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wakuu wa Shirika ikiwemo Bodi ya Wakurugenzi TANESCO ili kuhakikisha umeme wa uhakika na wa kutosha unapatikana.
 
Maazimio mengine muhimu waliyotoka nayo ni kuendelea kuimarisha mazingira  ya usalama wa wafanyakazi, wateja na raia pamoja na kulinda miundombinu ya Shirika,  kufanya kazi kwa juhudi na weledi katika kutimiza malengo ya Shirika na Serikali.
 
"Tuko tayari kutekeleza maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa hususani katika sekta ya nishati ya umeme yanafikiwa kwa mafanikio makubwa" amesema CPA Zawadia.
 
Vilevile CPA Zawadia alipongeza juhudi za Shirika katika kipindi cha mwaka 2020 na 2021 kwa kupiga hatua kubwa kwenye eneo la usambazaji wa huduma ya umeme. Licha ya mafanikio hayo ameutaka uongozi wa TANESCO kuweka mikakati itakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo wateja wanakutana nazo ikiwemo adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
 
Baraza kuu la wafanyakazi TANESCO liko kwa mujibu wa Sheria na hufanyika kila mwaka kwa lengo la kufanya tathmini ya kina ya haki, wajibu na maslahi ya wafanyakazi sambamba na kuweka mikakati itakayosaidia maendeleo ya ustawi Shirika.