Kijiji cha Kibwe Dodoma January 2022Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewahakikishia wananchi wa maeneo ya vijijini kuendelea kupata huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi elfu 27.
 
Hayo yamesemwa na Meneja Mwandamizi Kanda ya Kati, Mhandisi Frank Chambua leo Januari 15, 2022 katika Kijiji cha Kigwe Mkoani Dodoma, alipokuwa katika ziara ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa eneo hilo kuunganisha huduma ya umeme.
 
"Tumekuja hapa kuwahakikishia wananchi wa vijijini tunaendelea kuwaunganisha kwa bei ya shilingi elfu 27 kupitia miradi inayotekelezwa na TANESCO" amesema Mhandisi Chambua.
 
Alifafanua kuwa,Serikali  imefadhili miradi ya umeme kwenye maeneo ya vijijini hivyo wananchi wanatakiwa kulipia elfu 27 ambayo inajumuisha kodi ya ongezeko la thamani yaani (VAT).
 
Mkutano huo pia ulienda sambamba na elimu kwa wateja iliyohusu kuelimisha uma taratibu sahihi zinazotakiwa kufuatwa kwenye kupata huduma ya umeme.
 
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kusaidia kulinda miundombinu ya umeme hasa kipindi wanapoandaa mashamba na kuacha kuchoma nguzo moto.
 
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Bahi, Hassan A. Hassan amesema wanaendelea kuwaunganisha wateja wote wa maeneo ya vijijini kwa shilingi elfu 27.
 
"Tunaendelea kuwaunganishia wateja kwa elfu 27, leo tuna idadi ya wateja 16 ambao tutawaunganishia umeme, lakini pia tunahamasisha wananchi kuzidi kuomba kupata huduma ya umeme" amesema Hassan.
 
Kwa Mkoa wa Dodoma Serikali imewekeza jumla ya shilingi bilioni 195.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuunganisha umeme. Mkoa huo una jumla ya vijiji 581 ambapo mpaka sasa takribani vijiji 422 vimefikiwa na huduma ya  umeme na vilivyobaki ni 159 ambavyo wakandarasi wanaendelea na kazi ya kuunganisha huduma hiyo.