Malaraga1 for web siteShirika la umeme Tanzania TANESCO, linatarajia kuzalisha jumla ya megawati 49 ambazo zitaingia kwenye gridi ya taifa kupitia mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji kwenye maporomoko ya mto Malagarasi.
 
Hayo yameelezwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji uwekezaji wa TANESCO, Mhandisi Stephen Manda Februari 22, 2022 wakati wa ziara ya kuwaonesha wazabuni mbalimbali eneo utakapojengwa mradi wa Malagarasi Mkoani Kigoma.
 
"Lengo la kutukutanisha hapa ni suala zima la kuwaonyesha eneo la mradi wazabuni mbalimbali waliojitokeza kuomba zabuni ya mradi huu" alisema Mhandisi Manda.
 
Aliongeza kuwa kutakuwa na nafasi za ajira takribani 5000 ambapo asilimia 80 ya ajira za wafanyakazi katika mradi huo zitakuwa kwa ajili ya watanzania.
 
Naye Msemaji wa TANESCO, Martin Mwambene alisema mradi huo ni muhimu kwa ukanda wa Magharibi kwani utasaidia kuimarisha umeme kwnye gridi ya Taifa.
 
"Mradi huu utakapokamilika utaleta neema kubwa kwa wakazi wa Kigoma na hadi sasa Mkoa wa Kigoma unamatumizi ya megawati10 hivyo mradi huu utakua ni mkombozi kwa ziada ya miradi mingine inayozalisha umeme katika Mkoa wa Kigoma" alisema Martine.
 
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Malagarasi Mhandisi Victor Lutinah amesema utekelezaji wa mradi huo utakwenda sambamba na kuviunganishia huduma ya umeme kwenye vijiji ambavyo miundombinu ya umeme itapita.
 
Faida nyingine ni ujenzi wa barabara katika Kitongoji cha Igamba kijiji cha Mazumbwe ambako mradi wa Malagarasi unatekelezwa.
 

Mradi wa Malagarasi ni muhimu kwa ukanda wa Magharibi utatekelezwa kwa miezi 42 hadi kukamilika kwake na kugharimu takribani bilioni 400 ambapo utawezesha Mikoa ya Kigoma,Rukwa,Katavi na mikoa jirani kupata umeme wa uhakika na kuondokana na matumizi ya jenereta.