Mwenyekiti Kamati Machi 2022Kwa mara nyingine tena Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kupata pongezi za usimamizi mzuri wa miradi ya umeme nchini ambapo  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Nishati na Madini imesema kazi kubwa imefanyika ilipotembelea kukagua utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa kufua umeme kwa nguvu za maji wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha jumla ya megawati 2115.
 
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dunstan Kitandula ameyasema hayo leo Machi 16,2022 alipokua kwenye ziara ya  Kamati kukagua maendeleo ya wa mradi huo, ikiwa ni ziara ya kikanuni kutokana na kamati hiyo kuwa ndio yenye jukumu la kuisimamia Wizara ya nishati kwenye utendaji wa taasisi zilizo chini yake.
 
"Kimsingi kamati tumeridhika na kazi kubwa inayofanyika katika mradi huu, Tunaipongeza sana serikali  kwa jitihada inazozifanya kuhakikisha unakamilika na TANESCO kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi" amesema Mhe. Kitandula.
 
Kwa upande wake Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba amesema Wizara inaridhishwa na usimamizi mzuri wa TANESCO katika utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere.
 
"Tumefanya marekebisho kadhaa miezi michache iliyopita katika uendeshaji na usimamizi wa mradi na mabadiliko hayo yamesaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi katika kuhakikisha ubora na viwango vinazingatiwa,” amesema Waziri Makamba.
 
Aliongeza kuwa, dhamira ya Wizara ni kuhakikisha mradi wa Julius Nyerere unakamilika kwa viwango vinavyotarajiwa na watanzania ili uweze kuongeza uhakika wa upatikanaji nishati ya umeme nchini.
 
Akizungumzia maendeleo ya mradi Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande amesema mpaka sasa mradi umefika asilimia 56.84 kwa mujibu wa taarifa ya mwezi wa pili mwaka huu.
 
"Sina mashaka hata kidogo kwamba mradi utakamilika lililopo mbele yetu ni kufanya tathmini na kubuni mbinu za kupunguza muda wa ucheleweshaji hata ikitokea umechelewa basi iwe kwa siku chache iwezekanavyo kazi hiyo inafanyika kiuhandisi na tutafanya kazi usiku na mchana mpaka mradi ukamilike, " alimalizia Maharage.
 
Ziara hiyo ya kamati imekagua maendeleo ya mradi huo ikiwa ni moja ya jukumu lao la msingi kama kamati Katika kuhakikisha mradi unakamilika ili uweze kuchangia katika shughuli za kimaendeleo nchini.