KAMATI YA PIC KINYEREZIKamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji na mitaji ya umma leo Machi 28, 2022 imefanya ziara kukagua hatua za utekelezaji mradi wa upanuzi wa kituo cha Kinyerezi I na uzalishaji wa umeme kwenye kituo cha Kinyerezi II.
 
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Jerry Slaa, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi kubwa katika kuhakikisha miradi ya umeme inakamilika kwa wakati na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
 
 "Kukamilika kwa miradi kutapelekea nafuu kubwa ya hali ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa kawaida, viwanda na hivyo kukuza uchumi nchini " amesema Mhe. Slaa.
 
Ameongeza kuwa kufikia mwezi  wa nne mwaka huu mitambo miwili itawashwa kwa awamu ya kwanza ikifuatiwa na awamu ya pili ambayo itawashwa ifikapo mwezi wa nane na  kufikia mwezi wa kumi na moja mitambo yote sita itakuwa imeanza kazi na kupelekea hali ya umeme kuimarika kwa kiasi kikubwa.
 
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Stephen Byabato amesema mradi wa umeme wa upanuzi kituo cha Kinyerezi I unalenga kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa umeme kwa takribani asilimia 30 hadi 40.
 
“Tunatataka, tunatamani kuwa na umeme wa uhakika wa kutabirika na wa gharama nafuu” na pia mradi huu unatekelezwa kwa fedha za ndani kwa asilimia 100" ameongeza Mhe. Byabato.
 
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi wa upanuzi kituo cha Kinyerezi I kutasaidia katika mradi wa reli ya kisasa SGR ambapo kutakuwa na laini ya kujitegemea itakayotoka moja kwa moja katika kituo hicho hadi Kingolwira Morogoro kwenye kituo cha SGR.
 
Naye Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande ameishukuru Kamati pamoja na kusisitiza kuwa watafanya kazi bila kuchoka kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
 
Akiongelea matarajio kwenye uzalishaji Maharage amesema,ifikapo 2025 ni kiasi cha megawati 5000 kitazalishwa na megawati 18,000 ifikapo 2044.
 
"Kazi inayoendelea katika kituo cha Kinyerezi ni muendelezo wa kufikia malengo ambapo pindi mradi huo utakapo kamilika utaweza kuzalisha Megawati 185. Tuko kazini kuhakikisha tunatimiza malengo tuliyoahidi wananchi” Amesema Maharage.
 
Ziara hiyo ni mfululizo wa ziara za kamati za bunge kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)