Semina ya WabungeWizara ya nishati Mei 28  imefanya semina kwa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kuwajengea uelewa Waheshimiwa wabunge juu ya majukumu na shughuli zinazoendeshwa na Wizara pamoja na  taasisi zake.
 
Akifungua kikao hicho kilichofanyika Katika ukumbi wa treasury square ulioko jijini Dodoma Naibu waziri wa nishati Mh Stephen Byabato amesema semina hiyo ililenga kuwapa uelewa Waheshimiwa wabunge Kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara.
 
“Nawashukuru kwa kukutana leo na kuweza kuzungumza mambo mema yanayoendelea kutendeka ndani ya nchi hii yanayosimamiwa na wizara ya nishati na taasisi zake” amesema Byabato.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la umeme nchini TANESCO Maharage Chande alitoa wasilisho kuhusiana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika pamoja na kampuni zake tanzu katika kuongeza ufanisi wa utoaji huduma zake kwa wananchi.
 
Katika ufafanuzi wake juu ya hali ya umeme Maharage alieleza shughuli za shirika kuwa ni kuzalisha, kusafirisha umeme na kusambaza umeme ambapo kwa sasa kuna mitambo ya gesi na mitambo ya maji.
 
“ Kwa sasa uwezo wa kuzalisha umeme kwenye gridi ya taifa ni megawati 1694.35 kati ya hizo asilimia 87.47 ni uzalishaji wa sisi TANESCO na asilimia 12.53 ni uzalishaji unaofanywa na sekta binafsi”, amesema Maharage.
 
Semina hiyo ilihudhuriwa na wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Wizara ya nishati.