Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema mabadiliko ya katika taasisi za umma hayaepupikiki ilia kuleta ufanisi, akisema Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco), limeonyesha mfano katika mchakato huo.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anataka mageuzi ya kila taasisi za umma, akisema Ofisi ya Msajili ya Hazina watakuwa wakiangalia uongozi na nafasi ya za bodi katika utekelezaji wa majukumu yao.
"Pia watakuwa wakiangalia nafasi za bodi na menejimenti katika kufanya uamuzi kwa mujibu wa taratibu zao sambamba na kuwawezesha katika mitaji," amesema Mchechu.
" Tunategemea matokeo ya taasisi ni kutengeneza faida zitakazozalishwa na kuingizwa Serikalini au kujiendesha pasipo utegemezi wa Serikali kuu," amesema Mchechu aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 13, 2023 katika kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra (MTLF), kwa ushirikiano na Tanesco, mchakato uliokwenda sambamba na uzinduzi rasmi wa safari ya mabadiliko ya kuliangaza Taifa na ripoti ya mpango mkakati wa miaka 10 ya shirika hilo.
Mchechu amesema wamakubaliana kila taasisi za umma kutekeleza majukumu yao kwa uwazi ikiwemo kuwasilisha taarifa zao kwa wakati kuhusu utendaji wao ili kuwafanya wananchi kujua.
Katika hatua nyingine, Mchechu amesema bodi ya Tanesco itarudishiwa mamlaka yote ya kuendesha shirika hilo ikiwemo kuajiri sambamba na maslahi yao.Akisema Ofisi ya Msajili wa Hazina itakuwa ikiangalia vigezo vya utendaji kazi ili uhuru wao uendane na uwajibikaji.
" Hili litafanyika pia katika taasisi zenye mikakati mizuri kama ambavyo Tanesco ilivyo, lakini tutakwenda katika taasisi zote ili kuzipa uhuru.Tunatarajia kwa taasisi zingine viwango vilivyofanywa na Tanesco basi ndivyo vikubalike," amesema Mchechu.