loading...

LAZIMA TUWE NA VYANZO MBADALA VYA UMEME: Mhe. Doto Biteko  

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameweka jiwe la msingi katika mradi wa uzalishaji umeme jua wa Megawati 150 uliopo Kishapu Mkoani Shinyanga leo tarehe 14 Machi, 2024.

Mradi huu unatekelezwa ikiwa ni moja ya  mpango wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa kuongeza vyanzo mbadala vya uzalishaji umeme ili kuimarisha hali ya upatikanaji huduma ya umeme  kwa wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Kishapu katika hafla hiyo ameeleza kuwa mradi huu ni kati ya miradi mikubwa ya uzalishaji ya umeme iliopo hapa nchini na kuwa kukamilika kwake kutaimarisha hali ya umeme kwa Mkoa wa Shinyanga na Kanda ya Ziwa.

"Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu tunaendeleza mradi mkubwa wa umeme Jua wa Megawati 150 ambao kukamilika kwake kutaimarisha upatikanaji umeme katika Mkoa wa Shinyanga na Kanda ya ziwa kwa ujumla", ameeleza Mhe. Biteko.

Akieleza kuhusu vyanzo vya uzalishaji umeme vilivyopo sasa, amesema kuwa vyanzo hivyo vinatutosha kwa muda mfupi kwani vimekuwa vikiathiriwa na mabadiliko ya tabianchi hali inayopelekea kupata mgao wa umeme.

Pia ameongeza kuwa mradi huu wa umeme jua unatekelezwa kwa awamu mbili na utaanza kwa Megawati 50 awamu ya kwanza na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.

" Tumedhamiria kutumia vyanzo mbadala ya kuzalisha umeme ambavyo miaka mingi tumevisema lakini hatujaviendeleza. Tumeanza na mradi wa Kishapu wa umeme jua na tunaamini muda kama huu mwakani kutakuwa na mabadiliko na tumeanza kuzalisha Megawati 50 za umeme", ameeleza Mhe. Biteko.

Ameipongeza TANESCO kwa juhudi na usimamizi mkubwa  katika kuhakikisha mradi huu unaanza mara moja kutekelezwa na kufikia lengo la kuwa na nishati mbadala ya umeme.

" Naipongeza sana TANESCO kwa usimamizi na kuharakisha mradi, bila nyie kuongeza spidi na kuusimamia kwa ukaribu usingefikia hatua hii iliyopo leo", amesema Mhe. Biteko.

Hafla hii imehudhuriwa na viongozi mbalimbali katika ngazi ya Mkoa na wabunge wa Mkoa wa Shinyanga ambao pia wamefurahishwa na namna mradi huu unavyotekelezwa kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa umeme.